Simbachawene aanza mkakati kuwachomoa wanaobambikiwa kesi

mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani  nchini Tanzania,  George Simbachawene amewataka watendaji wakuu wa Jeshi la Polisi kuwahoji  watuhumiwa waliopo mahabusu ili kujua tuhuma zinazowakabili, kama wanastahili kukaa rumande.

Amesema lengo ni kudhibiti watu kubambikiwa kesi jambo linalofanyika katika vituo mbalimbali vya polisi nchini, kwamba baadhi ya watuhumiwa wanapelekwa gerezani kwa makosa ambayo hawakuyafanya.

Akizungumza leo Jumatano Februari 19, 2020 katika kikao na watendaji  hao kilichofanyika  makao makuu ya jeshi hilo jijini Dar es Salaam, Simbachawene amesema hata Rais John Magufuli anajua kuhusu suala hilo.

“Nawataka mfanye mchujo katika kesi za watuhumiwa mbalimbali waliopo mahabusu  ambazo zinapelekwa mahakamani. Wafanyiwe ‘screening’ hata mara mbili au tatu kwa kuwahoji makosa yao uso kwa uso ili kuhakikisha mtuhumiwa huyo ndio mwenye kesi ya mauaji, ubakaji  au wizi, na hata akipelekwa mahakamani awe ndiye anayestahili.”

“Kunaweza kutokea wakati mwingine mtuhumiwa anakuwa na kesi nyingine lakini anapewa kesi ambayo hastahili na anashangaa kwa kuwa sio kosa alilolitenda,” amesema Simbachawene.

Kuhusu bodaboda

Amewataka watendaji wa jeshi hilo kusimamia kwa hekima na busara waendesha bodaboda ambao wengi ni vijana, akibainisha kuwa ni kundi kubwa lililojiajiri.

“Isitafsiriwe kwamba  bodaboda ni watu wa hovyo. Waendesha bodaboda wapo wenye shahada, stashahada, kidato cha sita na nne. Wenye vyeti wapo pia. Si watu wa hovyo kama wengi wanavyofikiria.”

“Hawa wamejiajiri wanafanya shughuli zao kihalali kwa mujibu wa sera za nchi, kwa hivyo ni lazima tutambue mchango wao na changamoto zao,” amesema Simbachawene.

Amesema lazima polisi watumie busara, uadilifu na kuwa na huruma kuwafuatilia waendesha bodaboda ambao wengi ni vijana.

“Duniani na nchini kuna ukosefu mkubwa wa ajira hivyo wanapotokea vijana wakajiajiri lazima eneo hilo litunzwe na lipendwe na sio kuchukuliwa kuwa eneo la kukomeshana kwa kuwanyanyasa na kuwafanya kama hawatakiwi katika jamii,” amesisitiza.

Sirro atoa neno

Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro amemshukuru Simbachawene kwa kukutana na watendaji hao, kumuahidi yote aliyeyasema watayatekeleza.

Simbachawene ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya uteuzi wa mtangulizi wake, Kangi Lugola kutenguliwa na Rais Magufuli.

Simbachawene ameanza ziara ya kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake.

#1 Downloaded Personalized News App

Read in App for better experience

cancel confirm